Vikosi hivyo vinajumuisha wanajeshi kutoka Kenya, Burundi, Sudan Kusini na Uganda.
- Author, Wafula & Kenneth Mungai
- Nafasi, BBC News, Nairobi
Baada ya kuhudumu kwa miezi 11 tu, kikosi cha Afrika Mashariki kilichoundwa ili kukabiliana na ghasia za wanamgambo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kimeamriwa kuondoka.
Serikali ya Congo ilisema haitaongeza muda wa Jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya miezi kadhaa ya Kinshasa kulalamikia kutofanya kazi kwa vikosi hivyo.
Uamuzi wa kutoongeza muda wa wanajeshi hao unakuja huku ghasia kati ya kundi la waasi la M23 na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali zikizuka katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa mara nyingine tena.
Je, jukumu la kikosi cha kikanda lilikuwa lipi?
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) – muungano wa nchi saba – ilituma wanajeshi wake DR Congo mwaka jana baada ya mapigano kuzuka upya kati ya majeshi ya serikali na waasi wa kundi la M23. Kikosi hicho kilikubaliwa muda mfupi baada ya DR Congo kujiunga na Jumuiya hiyo.
Kundi la M23 lililoundwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, limechukua udhibiti wa maeneo makubwa ya eneo la mashariki, likisema kwamba linafanya hivyo ili kutetea maslahi ya jamii ya Watutsi dhidi ya wanamgambo wa Kihutu ambao linasema wanaungwa mkono na serikali.
Burundi ilikuwa nchi ya kwanza kati ya nchi nne kutuma wanajeshi wake nchini DR Congo Agosti mwaka jana, ikifuatiwa na Kenya, Sudan Kusini na Uganda, huku Kenya ikiwa na kamandi ya jumla.
Jeshi la Kanda la EAC linasisitiza kuwa jukumu lake ni kusimamia uondoaji wa makundi yenye silaha kutoka maeneo yaliyotekwa.
Hata hivyo, serikali ya Congo na jumuiya za wenyeji wanataka jeshi hilo lishiriki katika mapambano ya moja kwa moja dhidi ya makundi kama vile M23.
Kikosi hicho kilianzishwa kufanya kazi pamoja na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa ambao tayari walikuwa nchini humo. Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, kinachojulikana kama Monusco, kimezidi kupoteza umaarufu kwa kushindwa kumaliza mzozo huo licha ya kuhudumu nchini humo kwa miaka 25. Rais Félix Tshisekedi alisema alianataka Monusco kujiondoa nchini humo mwezi Disemba.
Katika taarifa yake ya hivi karibuni, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilisema vikosi vyake vimejitolea kufanya kazi kwa karibu na serikali ili kuwezesha wakimbizi wa ndani kurejea katika makazi yao wakiwa salama na kuimarisha ulinzi wa raia kwa ujumla.
Mamlaka yake yameongezwa mara mbili tangu misheni hiyo ilipoanza.
Crédit: Lien source


Les commentaires sont fermés.